Katika sherehe hiyo iliyojaa nuru na mafunzo ya kiroho, Sheikh Maulana Hemedi Jalala alitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha amani, maelewano, na ushirikiano wa kidini nchini Tanzania, na kutunukiwa “Tuzo ya Amani na Heshima 2025”.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, ameshiriki katika hafla kubwa ya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) iliyofanyika usiku wa jana (Ijumaa: Tarehe 17-10-2025) katika Masjid Majmuuat Al-Islamiyyat, Temeke Mwisho - Dar es Salaam.
Hafla hiyo imeandaliwa kwa ustadi wa juu chini ya uongozi wa Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, ambaye ni Imam Mkuu wa Msikiti huo na Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Taifa (JMAT).
Tukio hilo lilihudhuriwa na wageni wa kitaifa na kimataifa, akiwemo Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, wawakilishi wa serikali, viongozi wa dini mbalimbali, na waumini kutoka sehemu mbalimbali za nchi.
Katika sherehe hiyo iliyojaa nuru na mafunzo ya kiroho, Sheikh Maulana Hemedi Jalala alitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha amani, maelewano, na ushirikiano wa kidini nchini Tanzania, na kutunukiwa “Tuzo ya Amani na Heshima 2025”.
Tuzo hiyo yenye heshima kubwa ilikabidhiwa kwake na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt.Abubakar Zubair bin Ally, ambaye pia alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo (akimiwakilisha Mheshimiwa Kasim Majaliwa - Waziri Mkuu wa Tanzania), akimpongeza kwa juhudi zake katika kukuza udugu wa dini na kuendeleza mafundisho ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) kwa njia ya hekima, upendo na uadilifu.
Kwa upande wake, Sheikh Jalala aliwashukuru waandaaji wa hafla hiyo, akisisitiza kuwa Maulid ni alama ya umoja na rehema, na akatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani, maridhiano, na heshima baina ya dini zote.
Hafla hiyo imeendelea kutajwa kama miongoni mwa Maulid bora zaidi nchini Tanzania mwaka 2025, ikiakisi sura halisi ya umoja wa Waislamu na mshikamano wa kijamii katika taifa hili la Tanzania lenye amani.
Your Comment